Umoja wa Mataifa wataka kuruhusiwa kuingia mkoani Tigray nchini Ethiopia bila vizuizi
2021-09-10 08:33:52| CRI

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imeipongeza Ethiopia kwa kuruhusu malori yaliyokuwa na misaada ya kibinadamu kuingia mkoani Tigray, na kutoa wito wa kuhakikisha misaada ya kibinadamu inapelekwa kaskazini zaidi mwa mkoa huo kila siku.

Ofisi hiyo imesema, kuanzia jumapili iliyopita, malori 150 yaliyobeba misaada ya kibinadamu yaliwasili Tigray, na kwamba malori karibu 100 yanatakiwa kuingia mkoani humo kila siku ili kuweza kukabiliana na mahitaji ya kibinadamu.

Hata hivyo, baadhi ya mahitaji, ikiwemo mafuta vilizuiliwa kuingia, na kusababisha operesheni za misaada kusimama na hazina ya chakula kumalizika.

OCHA imesema, karibu watu milioni 3.4 kati ya milioni 5.2 wanaohitaji zaidi msaada wamepokea msaada wa chakula kati ya mwezi Mei na Agosti mwaka huu. Ofisi hiyo imesema awamu nyingine ya msaada inatakiwa kuanza mapema ili kuhakikisha kuwa watu hao wana chakula kitakachowasaidia kuishi.