Sudan Kusini yaomba kutumia bandari ya Dar es Salaam ya Tanzania
2021-09-16 09:31:27| cri

Sudan Kusini jana iliiomba Tanzania iiruhusu kutumia bandari yake kuu ya Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya mawasiliano ya Ikulu, imesema ombi hilo la kutumia bandari ya Dar es Salaam lilitolewa wakati Albino Ayuel Aboug ambaye ni mjumbe maalumu wa rais Salva Kiir wa Sudan Kusini alipozungumza na rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania. Kwenye mazungumzo yao, Aboug amesema Sudan Kusini inataka kuingiza na kuuza bidhaa nje kupitia bandari ya Dar es Salaam, ambayo pia inazipatia huduma nchi nyingine zisizo na bahari kama vile Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kwa upande wa rais Hassan, amesema Tanzania iko tayari kuiruhusu Sudan Kusini kutumia bandari yake, ili kuisaidia nchi hiyo katika kukuza uchumi.