China yazitaka Marekani na Canada kuweka mpango wa utekelezaji wa haki za binadamu kwa mujibu wa kiwango cha kimataifa
2021-09-16 09:33:51| cri

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Bw. Zhao Lijian amesema, hadi sasa Marekani, Canada, Ufaransa, Ujerumani na Japan bado hazijaweka mpango wa kitaifa wa utekelezaji wa haki za binadamu, akizitaka nchi hizo ziweke mapema mpango huo kwa kufuata kiwango cha kimataifa, ili kulinda haki za binadamu za wananchi wao kwa vitendo halisi.

Bw. Zhao alisema hayo alipojibu maswali kuhusu haki za binadamu katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jana mjini Beijing.

Habari zinasema kuwa, balozi wa kudumu wa China katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa huko Geneva alihutubia Kikao cha 48 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kwa niaba ya takriban nchi 40, akizitaka nchi mbalimbali zitimize amani ya kudumu, kuhimiza na kulinda haki za binadamu.

Bw. Zhao amesema hotuba hii inawakilisha sauti ya haki na kimantiki ya jamii ya kimataifa, na kuonesha uwajibikaji wa China katika suala la haki za binadamu. Pia ameeleza kuwa hivi sasa ukiukwaji mbaya wa haki za binadamu unatokea kutokana na vita, migogoro na misukosuko ya kikanda, na maendeleo ya mambo ya haki za binadamu duniani yanakabiliwa na changamoto kubwa.