Algeria yafanya mazishi ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Bouteflika
2021-09-20 09:06:28| CRI

Algeria imefanya mazishi ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Abdelaziz Bouteflika, aliyefariki ijumaa akiwa na umri wa miaka 84.

Mazishi hayo yalifanyika jana mchana katika makaburi ya El- Alia kwenye uwanja wa mashujaa ambapo marais kadhaa wa zamani wamezikwa.

Rais Abdelmajid Tebboune, Waziri mkuu Aymene Benabderrahmane, na viongozi wengine waandamizi na wanafamilia walihudhuria mazishi ya Bouteflika.

Bendera nchini humo zilianza kupepea nusu mlingoti tangu jumamosi, na zitapepea kwa muda wa siku tatu kumkumbuka kiongozi huyo. Bw. Bouteflika aligombea urais wa Algeria mwaka 1999 na kupata ushindi mkubwa, na aliendelea kushinda vipindi vinne vya uchaguzi hadi mwaka 2019.

Mwaka 2013 alipata tatizo la ubongo lililomfanya apate matatizo ya kutembea na kushindwa kufanya kazi za urais ipasavyo.