Zanzibar yawatunuku madaktari wa China kutokana na kazi nzuri
2021-09-22 08:53:24| CRI

Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewatunuku nishani madaktari 21 wa kikundi cha matibabu cha China kwa kutambua mchango wao mzuri katika kutoa huduma za matibabu visiwani Zanzibar.

Rais Mwinyi amewatunuku madaktari hao kwenye hafla iliyofanyika katika Ikulu ya Zanzibar, baada ya kumaliza muda wao wa kutoa huduma kwa miezi 12 katika visiwa vya Zanzibar.

Rais Mwinyi ameishukuru Jamhuri ya Watu wa China kwa kuendelea kutuma vikundi vya madaktari Zanzibar tangu mwaka 1964, akisema vikundi hivyo vimesaidia sana katika kuimarisha mfumo wa afya wa Zanzibar, na kuokoa maisha ya mamia ya watu.

Amesema timu hiyo pia imesaidia katika mapambano dhidi ya janga la COVID-19, na kuongeza kuwa China pia imetoa chanjo kwa wafanyikazi walio mstari wa mbele, pamoja na wafanyikazi wa afya na wale wanaofanya kazi katika sekta ya utalii.

Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto wa Zanzibar Bw. Nassor Ahmed Mazrui, amesema madaktari bingwa 21 wa China walikuwa wanafanya kazi katika Hospitali ya Mnazi Mmoja ya Unguja, na Hospitali ya Abdulla Mzee ya Pemba.