Maonesho ya China na Afrika kuleta fursa mpya za ushirikiano
2021-09-28 11:45:47| Cri

Maonesho ya pili ya biashara na uchumi kati ya China na Afrika yamefunguliwa Jumapili, ambapo yanatarajiwa kuleta fursa mpya za ushirikiano kati ya pande mbili.

Maonesho hayo yatakayofanyika kwa siku 40, kwa njia ya mtandao wa internet na nje ya mtandao, na ambayo yamepewa kauli mbiu ya “Mwanzo Mpya, Fursa Mpya, na Mafanikio Mapya” yamevutia wafanyabiashara karibu 900 kutoka nchi 40 za Afrika na China, ambapo Algeria, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Afrika Kusini na Senegal ni nchi za heshima.

Akiongea kwenye sherehe ya ufunguzi naibu waziri wa biashara wa China Wang Bingnan amesema ushirikiano wa kiuchumi na kibisahara wa China na Afrika upo kwenye kipindi muhimu cha mabadiliko, kuboreshwa na kuongeza ubora na ufanisi.

Wakati maonesho hayo yakifunguliwa, maonyeshao mengine ya biashara ya kielektroniki kati ya China na Afrika nayo yamefanyika juzi huko Changsha.

Kupitia maonyesho hayo, bidhaa bora mbalimbali kutoka Afrika zimeingia kwenye familia za kawaida nchini China kupitia matangazo ya watu mashuhuri kwenye mtandao wa Internet. Bidhaa hizo ni pamoja na kahawa kutoka Ethiopia, ufuta kutoka Tanzania, pilipili nyeupe kutoka Cameroon, na divai nyekundu kutoka Afrika Kusini.

Hayo ni matangazo ya moja kwa moja ya kwanza kuhusu bidhaa za Afrika kwa pande zote katika historia, yaliunganisha raslimali za biashara, majukwaa ya biashara ya kielektroniki na njia za uuzaji. Pia maonyesho hayo yametoa mchango kwa kuzidisha ushirikiano wa kunufaishana kati ya China na Afrika na kujenga jumuiya yenye hatma ya pamoja kati ya pande hizo mbili.