Vikosi vya usalama vya Sudan vyazingira kundi la kigaidi katika mji mkuu
2021-10-05 10:30:32| CRI

Shirika rasmi la habari la Sudan, SUNA limesema kuwa vikosi vya usalama vya Sudan vimezingira ngome iliyopo katika eneo la makazi kusini mwa mji mkuu Khartoum, ambapo kundi la kigaidi limejificha.

Habari zimesema kuwa mapigano yalitokea jana Jumatatu kati ya vikosi vya usalama vya Sudan na kundi la kigaidi lililokuwepo katika eneo la makazi huko Jabra, hata hivyo hakuna taarifa zaidi za kina.

Wakati huohuo tovuti ya Sudan Tribune imenukuu chanzo cha polisi ikisema mapigano hayo makali yalisababisha kifo cha askari mmoja wa vikosi vya usalama, na wapiganaji kadhaa wa kundi hilo kukamatwa, wakiwemo wageni.

Habari zimeongeza kuwa hadi sasa, watu wasiopungua sita wa kundi hilo la kigaidi wamekamatwa, na vikosi vya usalama bado vinaendelea kumtafuta mwingine.