Somalia kushirikiana na UM kuinua kiwango cha huduma za afya ya akili nchini humo
2021-10-11 09:15:17| cri

Somalia na Umoja wa Mataifa Jumapili wiki iliyopita, ambayo ni Siku ya Afya ya Akili Duniani, zilitangaza kuunda kikosi kazi ili kuinua kiwango cha huduma bora za afya ya akili kwenye ngazi zote nchini humo.

Umoja wa Mataifa umesema Somalia imeathiriwa vibaya na changamoto ya afya ya akili kutokana na mgogoro uliodumu kwa miongo kadhaa na kusababisha karibu mmoja kati ya wasomalia watatu awe na tatizo la akili kwa kiwango fulani.

Waziri wa afya na huduma ya kibinadamu wa Somalia Fawziya Abikar Nur, amesema serikali itachukua hatua thabiti na kutoa huduma bora za afya ya akili nchini humo na anatarajia jamii inayosumbuliwa na matatizo hayo kuacha unyanyapaa dhidi yao na kutafuta msaada unaofaa, ili waweze kuzungumzia matatizo yao kwa njia ya wazi zaidi, kushughulikia mfadhaiko ipaswavyo na kuhimiza ustawi wa watu hao.

Amesema serikali ya Somalia ikishirikiana na Umoja wa Mataifa imeanzisha mkakati mmoja unaozingatia afya ya akili kwa mwaka 2019 hadi mwaka 2022 huku sera nyingine husika ikikaribia kuhitimishwa.