DRC yaripoti kuibuka tena kwa maambukizi ya Ebola kaskazini mashariki mwa nchi hiyo
2021-10-11 08:32:29| CRI

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC imethibitisha kesi mpya ya maambukizi ya virusi vya Ebola kaskazini mashariki mwa nchi hiyo, miezi mitano baada ya mlipuko uliopita wa Ebola kumalizika.

Wakati DRC inaendelea na mapambano makali dhidi ya janga la Corona, maafisa wa nchi hiyo Ijumaa iliyopita walithibitisha kuwa mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka mitatu alifariki kutokana na ugonjwa wa Ebola Jumatano iliyopita kwenye eneo la Beni, kaskazini mashariki mwa mkoa wa Kivu Kaskazini, eneo ambalo pia lilikuwa ni kiini cha mlipuko uliopita wa Ebola uliomalizika Mei 3.

Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Afya Duniani WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus alisema Jumamosi kupitia ukurasa wake wa Twitter, kuwa WHO inashirikiana na serikali ya DRC kwenye uchunguzi wa kesi mpya ya Ebola mkoani Kivu Kaskazini.