China na Kenya kuunganisha zaidi mikakati ya maendeleo na kuimarisha ushirikiano
2021-10-12 09:09:04| CRI

Waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Wang Yi amesema China itaendelea kushirikiana na Kenya kuimarisha kuunganisha mikakati ya maendeleo ya nchi hizo mbili na kuimarisha ushirikiano kati ya pande mbili kwenye sekta za mawasiliano, afya na elimu.

Akiongea kwa njia ya simu na mwenzake wa Kenya Bibi Raychelle Omamo, Bw. Wang amesema kutokana na mwongozo wa kimkakati wa marais wa nchi hizo mbili, uhusiano kati ya China na Kenya  umeendelea kuwa mzuri, licha ya janga la COVID-19.

Amesema China inapenda kuunganisha zaidi mikakati ya maendeleo ya nchi hizo mbili, na kushiriki kikamilifu kwenye mkakati wa ajenda kuu nne wa Kenya chini ya mpango wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, kuhimiza uendeshaji mzuri wa reli za SGR za Mombasa-Nairobi, na Nairobi-Malaba, na pia kuisaidia Kenya kufufua uchumi wake baada ya janga la COVID-19. Pia amesema China inaiunga mkono Kenya kuwa mwenyekiti wa zamu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Bibi Omamo ameishukuru China kwa msaada wake katika kupambana na janga la COVID-19, na kuhimiza maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini Kenya.