Afrika Kusini yazindua mkakati wa kuvutia watalii kutoka masoko lengwa
2021-10-13 09:07:16| CRI

Afrika Kusini imezindua mkakati wenye lengo la kuvutia watalii kutoka masoko yanayolengwa na nchi hiyo na kutarajia ongezeko katika kipindi cha sikukuu.

Mkakati huo ulipendekezwa na Wizara ya Utalii na idara nyingine za nchi hiyo, kufuatia kuenezwa kwa habari za upotoshaji kuhusu nchi hiyo katika sehemu mbalimbali duniani.

Waziri wa Utalii wa nchi hiyo Bibi Lindiwe Sisulu, amesema wataanza kutekeleza mkakati wa kuyalenga moja kwa moja masoko yao ili kuhakikisha wateja, wadau wa biashara na vyombo vya habari wanajua kuhusu utalii mzuri na wenye bei nafuu, rahisi na salama kwa wanaokwenda Afrika Kusini katika kipindi hiki cha COVID-19.

Amesema wameziarifu balozi za nchi hiyo kuhusu kazi zilizofanyika kwenye kupambana na COVID-19, na kutaka balozi hizo ziiambie dunia kuwa Afrika Kusini iko tayari kupokea watalii.

Hivi karibuni Afrika Kusini iliondolewa kwenye orodha nyekundu ya masoko makubwa ya utalii yakiwemo Marekani, Uholanzi, Uingereza na Ujerumani na kuipa msukumo sekta ya utalii ya nchi hiyo.