Uchafuzi wa hewa watajwa kuwa chanzo kikuu cha pili cha vifo barani Afrika
2021-10-18 14:33:16| CRI

Utafiti mpya unaonesha kuwa uchafuzi wa hewa umesababisha vifo vya watu milioni 1.1 barani Afrika katika mwaka 2019. Vingi vya vifo hivi 697,000 vilitokana na uchafuzi wa hewa wa ndani ya nyumba ambao kwa kiasi ulisababishwa na majiko ya kupikia.

Profesa wa Chuo cha Biolojia cha Boston, Philip Landrigan, ambaye ameongoza mradi na Pushpam Kumar ambaye ni Mchumi Mkuu wa Mazingira wa Shirika la Mpango wa Mazingira la Umoja wa Mataifa, amesema wakati uchafuzi wa hewa ndani ya nyumba ni aina kuu ya uchafuzi wa mazingira, sasa hivi unapungua kwani uchafuzi wa hewa kwenye mazingira ya nje unaongezeka, ukiashiria tatizo kubwa linaloendelea kukua.

Kwa mujibu wa ripoti, uchafuzi wa hewa ni chanzo kikuu cha pili cha vifo barani Afrika. Ni tishio kubwa kwa afya, mtaji wa binadamu, na maendeleo ya kiuchumi, na umesababisha asilimia 16.3 ya vifo vyote. Uchafuzi wa hewa wa mazingira ya nje unatokana na vyanzo kama moshi na uchafu unaotolewa viwandani ambao umesababisha vifo vya watu 394,000 barani humo. Uchafuzi wa hewa unasababisha vifo vingi kuliko tumbaku, pombe, ajali za barabarani na matumizi mabaya ya dawa. Isipokuwa Ukimwi unasababisha vifo vingi zaidi.