Sudan Kusini kuzindua kampeni ya upimaji wa COVID-19 nchi humo
2021-10-18 08:17:32| CRI

Serikali ya Sudan Kusini imesema jana kuwa inapanga kuzindua kampeni kubwa ya kupima virusi vya Corona na kutoa chanjo ili kudhibiti kuenea kwa virusi hivyo.

Kaimu msimamizi wa idara ya kukabiliana na COVID-19 nchini humo, John Rumunu amesema, upimaji wa umma utafanyika kwa kutumia vifaa vya utambuzi wa haraka ili kuweza kujua kiwango cha maambukizi nchini humo. Amesema kikosi kazi kimeamua kufanya mradi wa kutoa chanjo dhidi ya virusi hivyo katika maeneo yote ya umma na taasisi binafsi. Ameoongeza kuwa, hatua hiyo ni tahadhari kwa taasisi zote kuwa katika miezi michache ijayo, kusafiri nje ya nchi kutalazimu cheti kinachothibitisha kupata chanjo ya COVID-19.

Msimamizi wa janga la COVID-19 kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) Sacha Bootsman amesema, mpaka sasa ni asilimia 0.3 ya idadi ya watu nchini Sudan Kusini ndio wamepata chanjo ya COVID-19.