Kenya yaondoa marufuku ya kutembea usiku kufuatia kupungua kwa maambukizi na vifo vinavyotokana na COVID-19
2021-10-21 08:50:55| CRI

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ameamuru kuondolewa kwa marufuku ya kutembea usiku nchini humo ambayo iliwekwa tangu maambukizi ya COVID-19 yaliyotangazwa mwezi Machi mwaka jana, kufuatia kushuka kwa maambukizi na vifo vinavyotokana na virusi hivyo.

Akizungumza katika Siku ya Mashujaa iliyofanyika kitaifa katika Kaunti ya Kirinyaga, rais Kenyatta amesema marufuku hiyo imeondolewa kutokana na kupungua kwa tishio la janga hilo kwa uchumi na maisha ya watu.

Pia rais Kenyatta amesema, idadi ya watu wanaoweza kukusanyika katika nyumba za ibada imeongezwa kutoka theluthi moja hadi theluthi mbili, huku akisisitiza kudumishwa kwa hatua za kujikinga na maambukizi, ikiwemo kuvaa barakoa na kuweka umbali wa kijamii.

Aidha, rais Kenyatta amesema watu wazima milioni 5 wamepata chanjo dhidi ya COVID-19, lakini ameonya kuwa bado nchi hiyo haijabadili mwelekeo, hivyo kuwataka wananchi kuendelea kufuata hatua za kujikinga na maambukizi.