Wataalamu Nchi za Pembe ya Afrika wasema majadiliano ni ufunguo wa kuongeza ufadhili wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi
2021-10-22 08:59:12| CRI

Nchi za Pembe ya Afrika zimetakiwa kufanya mjadala wa pamoja wa kikanda wa kuongeza ufadhili katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika mkutano ujao wa hali ya hewa uliopangwa kufanyika mwezi ujao mjini Glasgow, Scotland.

Hayo yamesemwa na wataalamu wa nchi za kanda hiyo katika mkutano uliofanyika kwa njia ya video ambao uliandaliwa na Shirika la Maendeleo la Kiserikali la Nchi za Afrika Mashariki (IGAD) uliofanyika jijini Nairobi, Kenya.

Wataalam hao wamesema kuwa na msimamo wa pamoja katika mkutano wa hali ya hewa kutahakikisha kuwa nchi za Pembe ya Afrika zinapata fedha za kutosha na teknolojia zinazohitajika ili kuimarisha hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.