Serengeti yatajwa kuwa mbuga ya taifa bora
2021-10-22 11:39:16| CRI

Mbuga ya Taifa ya Serengeti ya Tanzania imetajwa kuwa mbuga ya taifa bora katika Afrika kwa kuzishinda nyingine sita za Afrika kwenye Tuzo za Dunia za Mashindano ya Utalii(WTA) kwa mwaka 2021.

Ikiwa maarufu kwa kuwa na msimu wa uhamaji wa Nyumbu na uwanda mkubwa wa mbuga wenye mamilioni ya wanyama pori wakiwemo wanyama wakubwa watano (Big 5), Serengeti imetajwa kuwa ni mbuga inayoongoza Afrika kwa mara ya tatu mfululizo. Serengeti iliingia kwenye kinyang’anyiro hicho na mbuga nyingine kama vile Hifadhi ya Central Kalahari ya Botswana, Mbuga ya Taifa ya Etosha ya Namibia, Mbuga ya Taifa ya Bonde Kidepo ya Uganda, Mbuga ya Taifa ya Kruger ya Afrika Kusini na Hifadhi ya Taifa ya Masai Mara ya Kenya.

Tuzo za WTA pia zimeitaja Kreta ya Ngorongoro na Mlima Kilimanjaro kuwa miongoni mwa maeneo ya kutembelea yanayoongoza katika Afrika, na kufanya mbuga tatu za taifa za Tanzania kuchukua nafasi kwenye orodha ya tuzo za uhifadhi za mwaka 2021.