Rais wa Uganda asema msako wa magaidi waliolipua mabomu hivi karibuni bado unaendelea
2021-10-26 09:10:19| cri

Rais wa Uganda Yoweri Museveni Jumatatu alisema msako wa magaidi waliofanya mashambulizi ya kulipua mabomu hivi karibuni bado unaendelea.

Kwenye twita yake Museveni alikuwa akijibu kuhusu mlipuko mpya uliotokea kwenye basi lililokuwa likisafiri kutoka Kampala kwenda sehemu za magharibi mwa nchi. Amesema polisi wanachunguza kama mtu aliyelipua bomu ndiye aliyebeba bomu au la, akibainisha kuwa ripoti za awali zinaonesha mlipuko ulitokea kwenye kiti na ulimuua mtu huyo pekee na kumjeruhi mtu aliyekaa nyuma yake. Ameendelea kufafanua kuwa abiria wengine 37 waliosalia pamoja na dereva wote walikuwa salama.

Awali polisi walisema watu wawili wameuawa kwenye tukio hilo na wengine kadhaa kujeruhiwa. Mlipuko huo umetokea siku kadhaa baada ya mlipuko wa bomu kwenye baa na mgahawa mjini Kampala uliosababisha mtu mmoja kuuawa na watatu kujeruhiwa. Polisi Jumatatu iliwataka watu kuwa macho na kuripoti tabia zozote zinazotia shaka.