Polisi ya Tanzania yakamata kilo 300 za bangi katika Ziwa Viktoria
2021-10-29 09:41:31| cri

Polisi ya Tanzania imesema Alhamisi kwamba imekamata kilo 300 za bangi katika Ziwa Viktoria na kuwatia nguvuni watuhumiwa watatu wanaohusishwa na bangi hizo.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Mwanza, Ramadhan Ng’anzi amesema washukiwa hao walikuwa wanasafirisha bangi iliyofungwa kwenye viroba saba na mifuko miwili ya plastiki kwenye boti. Amebainisha kuwa uchunguzi wa awali unaonesha kuwa bangi hiyo ilikuwa ikisafirishwa kutoka wilaya ya Tarime mkoani Mara na kupelekwa mkoa wa Mwanza kupitia ziwa.

Ng’anzi amesema watuhumiwa hao watatu watashtakiwa mahakamani kwa kuwa na dawa za kulevya kinyume na sheria baada ya uchunguzi unaohusisha mashirika kadhaa kukamilika.