Shirika la Afya Duniani (WHO) jana lilisema nchi 5 tu za Afrika zinatarajiwa kutimiza lengo la kuwapatia asilimia 40 ya wananchi wao chanjo za Corona ndani ya mwaka huu, ikimaanisha kuwa chini ya asilimia 10 ya nchi 54 za Afrika zinaweza kutimiza lengo hilo.
Ofisi ya WHO barani Afrika iliyoko mjini Brazzaville nchini Jamhuri ya Congo imesema, nchi tatu za Afrika zikiwa ni pamoja na Ushelisheli, Mauritius na Morocco zimetimiza lengo lililowekwa na Mkutano wa Afya Duniani mwezi Mei, ambapo Tunisia na Cape Verde pia zitatimiza lengo hilo.
WHO inaonya kuwa ukosefu wa fursa za kupata vifaa vikuu kama vile sirinji unaweza kupunguza kasi ya kupata chanjo za Corona barani Afrika. Baadhi ya nchi za Afrika zikiwemo Kenya, Rwanda na Afrika Kusini zimechelewa kupata sirinji.