Algeria kutathmini upya makubaliano ya ushirikiano na Umoja wa Ulaya
2021-11-01 10:47:11| CRI

Rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria amesema nchi yake itatathmini upya makubaliano ya ushirikiano na Umoja wa Ulaya. Taarifa iliyotolewa na rais huyo inasema uamuzi huo umefanywa kwenye mkutano wa baraza la mawaziri ulioongozwa na rais Tebboune.

Taarifa hiyo imesema rais huyo ameiamuru serikali kutathmini upya vifungu vyote vya makubaliano ya ushirikiano yaliyoanza kutekelezwa mwezi wa Septemba mwaka 2005.

Rais Tebboune amesisitiza kuwa mchakato wa kutathmini tena utafanywa kwa msimamo wa mamlaka na njia ya kunufaishana, huku ukizingatia maslahi ya Algeria.

Wakati huohuo, rais Tebboune ametangaza kusimamisha uuzaji wa gesi asili kwa Hispania kupitia Morocco, na kutoa taarifa ikiiamuru kampuni ya nishati ya taifa Sonatrach kusimamisha uhusiano wa kibiashara na Morocco, na kutorefusha mkataba wa bomba la gesi na nchi hiyo ulioisha usiku wa manane wa Oktoba 31 mwaka huu.