Takriban watu wanne wamefariki dunia baada ya jengo lenye ghorofa 21 lililokuwa likiendelea kujengwa kuporomoka Jumatatu mchana katika eneo la Ikoyi mjini Lagos nchini Nigeria.
Mratibu wa Shirika la Taifa la Usimamizi wa Mambo ya Dharura (NEMA) katika jimbo la Lagos, Ibrahim Farinloye amesema jengo hilo liliporomoka saa tisa mchana kwa saa za huko na hadi sasa miili ya watu wanne imepatikana na wengine wanne wameokolewa wakiwa hai. Farinloye amebainisha kuwa kipindi cha utafutaji na uokozi wa dharura kinaendela, ambapo wamepata usaidizi mwingine kutoka jeshi la Nigeria na kikosi cha anga, huku watu wengi zaidi wakihofiwa kukwama. Amesema chanzo cha jengo hilo kuporomoka bado hakijajulikana na uchunguzi unaendelea.
Wakati huohuo wakazi wanaoishi eneo hilo wamesema jengo hilo lipo kwenye ujenzi kwa zaidi ya mwaka mmoja, na zaidi ya watu 50, wengi wao wakiwa wajenzi wamekwama kwenye kifusi.