Tanzania yapokea dozi 500,000 za chanjo ya Sinopharm kutoka China
2021-11-02 14:55:56| CRI

Tanzania jana ilipokea shehena ya pili ya dozi 500,000 za chanjo ya Sinopharm kutoka China ambayo itaisaidia nchi hiyo kuongeza kasi ya kutoa chanjo kwa raia dhidi ya janga la COVID-19.

Mwanzoni mwa mwezi Oktoba Tanzania ilipokea dozi milioni 1.065 za chanjo ya Sinopharm kutoka serikali ya China kwa kupitia mpango wa COVAX.

Akiongea mara baada ya kupokea chanjo hizo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wa Tanzania Bibi Dorothy Gwajima, aliishukuru serikali ya China kwa kutoa misaada kwa wakati, akisema kuwa chanjo hizo zitaisaidia sana Tanzania kupambana na janga la COVID-19.

Bibi Gwajima alitoa wito kwa Watanzania kwenda kuchoma chanjo ya Sinopharm, akisema chanjo hiyo ni salama na zimeidhinishwa na Shirika la Afya Duniani.