Mafundi zaidi ya 1,500 kushiriki kwenye meonesho ya kampuni ndogo na za wastani za jumuiya ya EAC
2021-11-03 09:38:02| CRI

Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC imetoa taarifa ikisema, mafundi zaidi ya 1,500 watashiriki kwenye maonesho ya awamu ya 21 ya kampuni ndogo na za wastani MSMEs ya jumuiya hiyo yatakayofanyika Mwanza Tanzania.

Maonesho hayo yenye kaulimbiu ya “kuhimiza ubora na uvumbuzi ili kuimarisha ushindani wa kampuni za EAC na ufufukaji wa uchumi baada ya maambukizi ya COVID-19” yatafanyika kuanzia Desemba 2 hadi 12, na kushirikisha mafundi zaidi ya 1,500 kutoka nchi wanachama wa jumuiya ya EAC zikiwemo Burundi, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Tanzania na Uganda.

Taarifa hiyo imesema, maonesho ya kwanza ya MSMEs yalifanyika mwaka 1999 mkoani Arusha, Tanzania, wakati makubaliano ya kuanzisha jumuiya ya EAC yakisainiwa. Baada ya maonesho kupata mafanikio, viongozi wa jumuiya hiyo wameelekeza kufanyika kwa maonesho hayo kwa zamu katika nchi wanachama, ili kuhimiza na kuboresha mafungamano ya kiuchumi na kijamii ya watu wa Afrika Mashariki.