Ethiopia yatangaza sheria ya hali ya dharura katika nchi nzima
2021-11-03 09:22:09| CRI

Serikali ya Ethiopia jana Jumanne ilitangaza sheria ya hali ya dharura nchini kufuatia kuongezeka kwa mgogoro kaskazini mwa nchi hiyo.

Uamuzi huo ulitolewa na Baraza la Mawaziri la Ethiopia, ambao unatarajiwa kupitishwa na Baraza la Wawakilishi la Ethiopia katika siku mbili zijazo. Hali ya dharura itaendelea kutekelezwa kwa miezi sita.

Naye katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameeleza wasiwasi mkubwa kuhusiana na vurugu zilizoongezeka katika siku za karibuni, pamoja na hali ya dharura iliyotangazwa na nchi hiyo.  Kwenye taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Bw. Guterres amerejea tena wito wake wa kuacha uadui mara moja na kuondoa vizuizi vya misaada ya kibinadamu ili kufikisha misaada hiyo kwenye mikoa yenye vurugu ya kaskazini.

Bw. Guterres pia ametaka kufanyika kwa mazungumzo jumuishi ya taifa ili kutatua mgogoro huu na kuweka msingi wa amani na utulivu katika nchi nzima.