Mwenyekiti wa Kamati ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat jana alieleza wasiwasi wake mkubwa juu ya kuongezeka kwa makabiliano ya kijeshi nchini Ethiopia, na kutaka kusitishwa uadui mara moja, kuheshimu maisha na mali za raia, pamoja na miundombinu ya taifa.
Bw. Mahamat pia amezitaka pande zote za mgogoro kufanya mazungumzo na kutafuta ufumbuzi wa amani kwa ajili ya maslahi ya nchi.
Wakati huohuo serikali ya Ethiopia imethibitisha kufanya mashambulizi ya anga yaliyowalenga waasi katika mkoa wa Tigray. Kwenye taarifa iliyoyotolewa na Huduma za Mawasiliano za Serikali, kikosi cha anga kililenga kituo cha mafunzo ya kijeshi cha Adi Bukray ambacho ni kwa ajili ya kundi la kigaidi la TPLF kilichopo karibu na Adi Hageray. Taarifa imesema idadi kubwa ya watu walioandikisha kinyume cha sheria wanapatiwa mafunzo kwenye kituo hicho.
Tangu mapema Novemba 2020, serikali ya Ethiopia imekuwa ikifanya operesheni ya Kijeshi dhidi ya TPLF.