Rwanda na China zaadhimisha miaka 50 ya uhusiano wa kidiplomasia
2021-11-09 08:56:34| cri

Rwanda na China zimeadhimisha miaka 50 tangu kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili, ikiashiria mafanikio makubwa na pia kuweka jukwaa la kutafuta maeneo mapya ya ushirikiano kati yao.

Akizungumza katika hafla ya maadhimisho hayo iliyofanyika mjini Kigali, Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Rwanda Vincent Biruta ameishukuru serikali ya China kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Rwanda kwenye sekta muhimu ikiwemo uwekezaji, miundombinu, TEHAMA, madini, afya na kilimo.

Waziri huyo amerejea utayari wa Rwanda wa kutafuta njia mpya za kuongeza uhusiano wa kina kati ya nchi hizo mbili chini ya mifumo iliyoko sasa ya pande mbili na pande nyingi.

Balozi wa China nchini Rwanda Rao Hongwei amesema, katika kipindi hicho cha miaka 50, nchi hizo mbili zimedumisha kiwango kikubwa cha kuaminiana, na kufanya uhusiano wa pande mbili kuwa wa utulivu licha ya mabadiliko ya mazingira ya kimataifa.