Jeshi la Rwanda lakana kuhusika na vitendo vya waasi wa kundi la M23
2021-11-10 08:32:15| CRI

Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) limekana tuhuma za kuunga mkono mashambulizi yaliyofanywa na kundi la waasi la M23 jumapili katika mpaka wa kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Uganda.

Katika taarifa yake iliyotolewa jana jumanne, Jeshi hilo limesema, imeripotiwa kuwa kundi lenye silaha linaloaminiwa kuwa waasi wa kundi la zamani la M23, walivuka mpaka na kuingia nchini DRC wakitokea Uganda ambako ni maskani yake, na kushambulia na kukalia vijiji vya Tishanzu na Runyoni.

Taarifa hiyo imesema, Jeshi la Rwanda halihusiki wala kuunga mkono vitendo vyovyote vya kundi la zamani la M23, na kuongeza kuwa, kundi hilo halikutafuta hifadhi nchini Rwanda lilipotoka nchini DRC mwaka 2013, lakini limekuwa na makazi yake nchini Uganda.