China na Misri zasaini makubaliano ya ushirikiano wa uchumi na teknolojia
2021-11-10 08:30:18| CRI

Balozi wa China nchini Misri Liao Liqiang na waziri wa ushirikiano wa kimataifa wa Misri Rania Al-Mashat kwa niaba ya serikali za nchi zao, wamesaini makubaliano ya ushirikiano wa uchumi na teknolojia.

Bw. Liao Liqiang amesema, chini ya msingi wa ushirikiano kati ya China na Afrika na kujenga kwa pamoja “Ukanda Mmoja, Njia moja”, China na Misri zimehimiza maendeleo na ushirikiano katika sekta ya matibabu na afya, elimu, mawasiliano, upashanaji wa habari na sekta ya anga za juu, na kutekeleza kwa pamoja miradi mbalimbali ya ushirikiano na kupata matokeo makubwa. Amesema China inapenda kushirikiana na Misri kuongeza juhudi katika kuharakisha utekelezaji wa ajenda ya maendeleo endelevu ya mwaka 2030 ya Umoja wa Mataifa na kutimiza maendeleo endelevu ya dunia nzima.

Bibi Al-Mashat amesema Misri inashukuru China kwa kuiunga mkono na kutoa msaada kwa maendeleo ya uchumi na jamii ya Misri, hasa katika wakati wa janga la COVID-19. Ameongeza kuwa Misri inatumai kujifunza uzoefu wa maendeleo ya China, kuingiza teknolojia ya kisasa ili kuhimiza maendeleo ya uchumi na jamii nchini na kuongeza maslahi ya watu wake.