Tanzania yapanga kujenga mabwawa manne ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi
2021-11-11 08:23:36| CRI

Tanzania inapanga kujenga mabwawa manne ya kimkakati katika maeneo tofauti ya nchi hiyo ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza na wanahabari mjini Dodoma, Waziri wa Maji nchini humo Jumaa Aweso amesema, maandalizi yanaendelea kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa hayo ya kimkakati katika mikoa ya Dodoma, Morogoro, Songwe na Iringa, na kuongeza kuwa ujenzi huo utaenda sambamba na ujenzi wa mabwawa ya ukubwa wa kati katika maeneo kadhaa nchini humo.

Amesema mabadiliko ya tabianchi yameathiri sana vyanzo vya maji nchini Tanzania, na hatua nyingine zinazochukuliwa kukabiliana na athari hiyo ni pamoja na kuvuta maji kutoka Ziwa Viktoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa, na pia kuvuta maji kutoka kwenye mito mikubwa ya Ruvuma, Rufiji, Kiwira, Songwe na Kagera.