Rais mzungu wa mwisho Afrika Kusini FW de Klerk afariki dunia, aomba radhi kwa ubaguzi wa rangi
2021-11-12 10:26:14| Cri

Rais mzungu wa mwisho nchini Afrika Kusini, FW de Klerk amefariki dunia jana Alhamis akiwa na umri wa miaka 85 baada ya kuugua saratani.

De Klerk na rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini Nelson Mandela wote wawili walipata tuzo ya Nobel ya amani mwaka 1993 kwa kuleta mabadiliko ya "muujiza" kutoka utawala wa wazungu. FW de Klerk ameacha mke Elita na watoto wawili Jan and Susan.

Rais huyo wa zamani aliingia madarakani mwaka 1989, nafasi ambayo aliendelea nayo hadi alipokabidhi utawala kwa Mandela baada ya uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia mwaka 1994.

Saa chache tu baada ya kifo chake ilitolewa video na mfuko wake, ikimuonesha FW de Klerk, akiomba radhi kwa vitendo vya ubaguzi wa rangi vilivyofanywa na utawala wa wazungu. De Klerk amesema anaomba radhi kwa binafsi yake na vilevile kama rais wa zamani wa Chama cha National Party, ambacho kilianzisha mfumo mkali wa ubaguzi wa rangi.