Rais wa zamani wa Afrika Kusini FW de Klerk kutofanyiwa mazishi ya kitaifa
2021-11-15 09:08:56| CRI

Mfuko wa FW de Klerk ulioanzishwa na rais wa mwisho wa utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, Frederik Willem (FW) de Klerk, ulitangaza Jumapili kwamba shughuli ya kuuchoma mwili na mazishi ya hayati de Klerk, itafanyika Novemba 21, ikishirikisha familia tu, na vyombo vya habari havitaruhusiwa.

Kwa mujibu wa mwongozo rasmi wa polisi kuhusu mazishi uliotangazwa na ofisi ya rais, marais wa zamani wa Afrika Kusini wana haki ya kufanyiwa mazishi ya kitaifa. Lakini, mpango wa mazishi ya de Klerk, aliyefariki Alhamis wiki iliyopita nyumbani kwake Cape Town baada ya kuugua saratani, umezua mjadala mkubwa tangu kutangazwa kifo chake.

Kuna wanaosema kwamba de Klerk, hapaswi kufanyiwa mazishi ya kitaifa kwani alikuwa rais wa utawala wa ubaguzi wa rangi, ambapo watu weusi wengi waliteseka, na kwenye mahojiano ya mwaka 2020 hakukubali kwamba ubaguzi wa rangi ni uhalifu dhidi ya binadamu, lakini baadaye alibadili kauli na kuomba radhi.