Mtaalamu wa Nigeria: Njia ya China kuhimiza ustawi wa pamoja miongoni mwa watu wake yastahili kuigwa na nchi nyingine zinazoendelea
2021-11-17 08:33:45| CRI

Mtaalamu wa Nigeria: Njia ya China kuhimiza ustawi wa pamoja miongoni mwa watu wake yastahili kuigwa na nchi nyingine zinazoendelea_fororder_李坤资料照片

Mtaalamu kutoka Nigeria katika Taasisi ya Utafiti wa Afrika ya Chuo Kikuu cha Ualimu cha Zhejiang, China Dkt. Adekunle Osidipe amesema,“kila mara anapoona vyombo vya habari vya magharibi vinapotosha ukweli na kuichafua China, siku zote ana hamu kubwa ya kutoa mchango wake katika kuifahamisha dunia hali halisi kuhusu China.”

Alipohojiwa hivi karibuni na Shirika Kuu la Utangazaji la China CMG, Dkt. Osidipe amesema China ikiwa ni mshirika mkuu wa Afrika kwenye biashara na maendeleo, vyombo vya habari vya magharibi siku zote vimekuwa vikiendeleza kampeni ya propaganda hasi dhidi ya China, vikijaribu kuichafua sura ya China miongoni mwa waafrika. Anaona Afrika na China zinapaswa kuimarisha ushirikiano kati ya vyombo vya habari, ili kuongeza kwa pamoja sauti za kuelezea mambo ya Afrika na China.

Tangu alipokuwa na mawasiliano na China kwa mara ya kwanza mwaka 2005, Dkt. Osidipe amekuwa na uelewa wa kina zaidi kuhusu China. Mwanzoni ufahamu wake kuhusu China ulitokana na taarifa za upande wa tatu na filamu za zamani za China, ambao ni tofauti kabisa na hali halisi anayoshuhudia mwenyewe nchini China. Amesema, “China ni nchi iliyoendelea zaidi, ya kisasa zaidi na iliyo wazi zaidi kuliko alivyofikiria”.

Dkt. Osidipe ameishi na kufanya kazi mjini Jinhua katika mkoa wa Zhejiang kwa miaka mingi, mkoa ambao uliteuliwa na serikali kuu kujenga Eneo la Mfano la Ustawi wa Pamoja. Amesema China imefanikiwa kutokomeza umaskini uliokithiri, na kuendelea kuwezesha ustawi wa maeneo ya vijijini. Aliwahi kutembelea baadhi ya maeneo ya vijijini mkoani Zhejiang, ambayo yamejengwa kama “miji midogo” yenye mifumo kamili ya miundombinu kama vile umeme, maji, mtandao na barabara. Dkt. Osidipe anaona China inajitahidi kuhimiza ustawi wa pamoja miongoni mwa wananchi wake, kuendelea kupunguza pengo kati ya matajiri na maskini, na kuwasaidia watu wenye kipato cha chini kuongeza mapato yao, hatua ambazo zitaimarisha kwa kiasi kikubwa utulivu na ustawi wa jamii. Amesema hatua hizo za China zinastahili kuigwa na nchi nyingine zinazoendelea.