Mapato ya mauzo ya nje ya Kenya yameongezeka kufuatia kulegezwa vizuizi vya COVID-19 katika masoko ya nje
2021-11-17 10:25:50| CRI

Shirika la Kukuza Usafirishaji Bidhaa na Chapa la Kenya (KEPROBA) limesema Kenya imerekodi ongezeko la asilimia 15.6 katika mauzo yake ya jumla ya nje ndani ya kipindi cha mwezi Januari hadi Agosti, ambayo ni Shilingi bilioni 490 sawa na dola bilioni 4.37 za Marekani, kutoka dola bilioni 3.78 zilizorekodiwa katika kipindi kama hicho mwaka jana.

KEPROBA imesema ongezeko la mapato ya usafirishaji nje linatokana na juhudi za nchi kupunguza utegemezi kwenye masoko tete ya kilimo.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Wilfred Marube amebainisha kuwa kulegezwa kwa vizuizi vya COVID-19 katika masoko wanayosafirisha bidhaa zao pia kumesaidia ongezeko la mapato hayo. Amesema Kenya inajaribu kubadilisha mauzo yake ya nje, ambapo bidhaa muhimu zinazosafirishwa nje ni pamoja na maua, chai, mavazi na nguo, kahawa, madini, bidhaa za mafuta ya petrol, mafuta ya wanyama na mimea, mashine na vipuri, bidhaa za chuma pamoja na dawa.