EAC yakaribia kukamilisha ahadi ya ushuru ili kufuata ushuru wa AfCFTA
2021-11-18 09:27:24| CRI

EAC yakaribia kukamilisha ahadi ya ushuru ili kufuata ushuru wa AfCFTA_fororder_东非

Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC imetoa taarifa ikisema imepiga hatua katika kufuata mahitaji ya biashara chini ya Eneo la Biashara Huria la Afrika (AfCFTA) huku mipango ikiendelea kukamlisha ahadi ya ushuru.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji la Afrika Mashariki (SCITFI) limeielekeza sekretarieti ya EAC kuitisha mikutano na wataalamu hadi kufikia Disemba 15, 2021, ili kukamilisha ahadi ya ushuru wa EAC. Aidha inatakiwa pia kufanya tathmini ya idadi ya mistari ya ziada ya ushuru ambayo imeondolewa na kila nchi mwanachama kwenye vitengo mbalimbali.

Katibu Mkuu wa sekretarieti ya EAC Peter Mathuki, amesema mambo mengi yanahitajika kufanywa ili kuanzisha biashara chini ya makubaliano ya AfCFTA. Ameongeza kwamba EAC ina nia ya kutekeleza sera, maamuzi na maelekezo ili kurahisisha biashara chini ya makubaliano yaliyowekwa na kupanua mafungamano pamoja na kuongeza biashara ya ndani ya bara la Afrika.