Azimio la kisiasa lasainiwa nchini Sudan baada ya msukosuko wa mwezi mmoja
2021-11-22 09:02:35| CRI

Azimio la kisiasa lasainiwa nchini Sudan baada ya msukosuko wa mwezi mmoja_fororder_苏丹 头图

Karibu mwezi mmoja baada ya kutokea kwa msukosuko wa kisiasa nchini Sudan, Kamanda mkuu wa majeshi ya Sudan Jenerali Abdel Fattah Al-Burhan na waziri mkuu aliyeondolewa madarakani Bw. Abadalla Hamdok wamesaini azimio la kisiasa linalohusisha kuteuliwa tena kwa Bw. Hamdok kuwa waziri mkuu.

Sudan imekuwa kwenye msukosuko wa kisiasa tangu Jenerali Al-Burhan kutangaza hali ya hatari Oktoba 25 na kuvunja baraza lenye mamlaka na baraza la mawaziri. Tarehe 11 Novemba Jenerali Al-Burhan alitoa amri ya kikatiba kutangaza kuundwa kwa baraza la mpito lenye mamlaka, na kujitangaza yeye kuwa mwenyekiti wa baraza hilo. Tangu wakati huo maandamano kadhaa yalitokea kupinga hatua za jenerali huyo.

Azimio jipya limetaja kuwa katiba itakuwa ni mwongozo wa kipindi cha mpito, na kuhakikisha ushiriki mpana wa kisiasa, isipokuwa chama cha Congress cha aliyekuwa rais wa Omar al-Bashir kilichoondolewa madarakani. Azimio hilo pia limeahidi kufanya uchunguzi wa mauaji na majeruhi ya raia na wanajeshi kwenye maandamano ya hivi karibuni, na kukamilisha uundaji wa taasisi za mpito.

Mwenyekiti wa kamati ya Umoja wa Afrika Bw. Moussa Faki Mahamat amepongeza kusainiwa kwa azimio hilo, na kuitaja kuwa ni hatua muhimu ya kurudi kwenye utaratibu wa katiba kama ilivyotajwa kwenye makubaliano ya Khartoum ya Agosti 19, 2019 yaliyoweka msingi wa masikilizano ya kisiasa na mpito kuelekea kwenye demokrasia. Amewakumbusha wadau wote wa Sudan kutekeleza azimio hilo kwa njia shirikishi na yenye ufanisi, kwenye mazingira ya amani na masikilizano ya kitaifa.

Kufuatia kusainiwa kwa azimio hilo, Jenerali Al-Burhan ameutaka Umoja wa Afrika kuirudisha Sudan kwenye uanachama wa umoja huo. Amesema hayo kwenye mkutano na naibu waziri mkuu na waziri wa mambo ya nje wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Bw Christophe Lutundula Apala, ambaye nchi yake ni mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Afrika. Bw. Apala ameitaja hatua ya Sudan kuwa ni ya kihistoria baada ya kuteleza kidogo kwenye mpito wake kuelekea demokrasia.