Balozi wa Tanzania aeleza matumaini yake kwa mkutano wa FOCAC utakaofanyika nchini Senegal
2021-11-23 14:35:54| Cri

Balozi wa Tanzania nchini China Mbelwa Kairuki, ameeleza matumaini yake kwa Mkutano wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika FOCAC utafanyika wiki ijayo huko Dakar, Senegal.

Balozi Kairuki amesema mkutano huo unafanyika katika kipindi ambacho dunia inakabiliana na janga la COVID-19, mabadiliko ya tabianchi na uhaba wa chakula. Amesema anatarajia kwamba, kupitia jukwaa la FOCAC, masuala hayo matatu yatakuwa ni msingi wa ushirikiano katika miaka ijayo, na China na Afrika zitashirikiana katika eneo la afya, utaalamu, vifaa pamoja na uwekezaji wa viwanda ambavyo vitazalisha vifaa tiba.

Kwa upande wa mabadiliko ya tabianchi, Balozi Kairuki amesema anatumai kuwa China na Afrika zitashirikiana katika kubadilishana uzoefu, kuchukua hatua za pamoja zitakazohakikisha mabadiliko ya tabianchi hayatakuwa na athari kubwa kwa nchi za Afrika na China.

Kuhusu uhaba wa chakula, Balozi huyo amesema China ni nchi ambayo watu wengi wanahamia mijini, huku shughuli za kilimo zikipungua, hivyo Afrika ina nafasi nzuri ya kuzalisha chakula cha kutosha kwa ajili ya soko la China, lakini kikubwa kinachohitaji teknolojia kutoka China, kwa ajili ya kuongeza thamani ya bidhaa za Afrika, ili ziuzwe kwenye soko la China.

Balozi Kairuki pia anatarajia kuwa China itaendelea kutoa mikopo kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu kwa nchi za Afrika, kwa kuwa miundombinu ni msingi wa maendeleo, na itawezesha shughuli za uchumi kufanyika kwa ufanisi zaidi

Pia amesema anatumai kuwa China itaendelea kuwezesha makampuni madogo ya Afrika kupata mitaji kwa ajili ya kununua teknolojia mbalimbali za uzalishaji, hususan za kuongeza thamani kutoka China, ili bidhaa za Afrika zitakazoongezewa thamani ziweze kupata soko kubwa zaidi.