UM wawahamisha ndugu wa wafanyakazi wake kutoka Ethiopia
2021-11-24 08:47:53| CRI

Msemaji wa Umoja wa mataifa Bw. Stephane Dujarric amesema Umoja wa Mataifa unawaondoa ndugu wa wafanyakazi wake kutoka Ethiopia kutokana na kuwepo kwa vurugu.

Bw. Dujarric amesema kutokana na hali ya usalama ya hivi sasa nchini Ethiopia, na tahadhari inayondelea kuwepo, Umoja wa Mataifa umeamua kupunguza uwepo wake nchini humo kwa muda na kuwahamisha ndugu wote wa wafanyakazi wake, lakini wafanyakazi wake wataendelea kutekeleza majukumu yao.

Eneo la kaskazini mwa Ethiopia limekumbwa na vurugu tangu mwaka jana, na sasa vurugu hizo zimeenea hadi mashariki kwenye jimbo la Afar na kusini kwenye jimbo la Amhara.

Mjini Addis Ababa wafanyakazi kadhaa wa umoja huo walikamatwa na serikali, na madereva 70 wanaofanyakazi kwa mkataba kwa ajili ya Umoja huo pia walikamatwa.