Mwanahabari wa Jamhuri ya Kongo: China imefanikisha mambo yasiyowezekana
2021-11-25 10:46:37| CRI

Mwanahabari wa Jamhuri ya Kongo: China imefanikisha mambo yasiyowezekana_fororder_Liwata

Mwandishi wa habari kutoka Jamhuri ya Kongo, Brinel Liwata hivi karibuni amesema, kilicholetwa na Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika ni uhai wa mawasiliano, miradi inayonufaisha umma na matokeo yanayoboresha maisha ya watu.

Akihojiwa na Shirika Kuu la Utangazaji la China (CMG), Bw. Liwata ambaye anasomea masomo ya diplomasia katika Taasisi ya Utafiti wa Afrika ya Chuo Kikuu cha Ualimu cha Zhejiang, amepongeza mchango mkubwa wa China katika kuboresha miundombinu barani Afrika. Amesema, watu wanapozungumzia barabara katika Jamhuri ya Kongo, cha kwanza wanachofikiria huwa ni China, kwa sababu China imefanikisha mambo yasiyowezekana. Akitolea mfano wa barabara Namba 1, amesema barabara hiyo iliyojengwa na kampuni ya China imetimiza ndoto ya watu wa Jamhuri ya Kongo. Kwa muda mrefu, njia muhimu ya kiuchumi kutoka Brazzaville hadi Pointe-Noire, ilikuwa inategemea tu reli ya Congo-Ocean iliyojengwa wakati wa ukoloni. Kujenga barabara kati ya maeneo hayo mawili ilikuwa ni mradi usiowezekana ambao unatakiwa kupita kwenye maeneo yenye hali ngumu za kijiolojia kama vile misitu ya asili ya Mayombe. Lakini wajenzi wa China walitumia stadi zao za hali ya juu kukamilisha mradi huo mgumu wa barabara yenye urefu wa kilomita 500, ambayo ilizinduliwa rasmi mwaka 2016. Bw. Liwata amesema, barabara hiyo imeinua kwa kiasi kikubwa uwezo wa usafiri wa barabara nchini Jamhuri ya Kongo.

Mbali na barabara hiyo, kampuni za China pia zimejenga viwanja vya ndege, madaraja, hospitali na shule, na kujitokeza kuwa mkandarasi mkuu wa miradi ya ujenzi nchini Jamhuri ya Kongo. Bw. Liwata amesema, wakati nchi yake ilipopata uhuru mwaka 1960, urefu wa jumla wa barabara katika nchi nzima ulikuwa ni kilomita tano tu, lakini hivi sasa urefu wa barabara za lami nchini humo umefikia kilomita 3,111, maendeleo hayo yanamaanisha kuwa wakazi wa eneo la kusini zaidi nchini humo wanaweza kufika eneo la kaskazini kabisa la nchi hiyo ndani ya siku moja, jambo ambalo zamani lilikuwa haliwezekani. Amesema, kutokana na maendeleo ya barabara, sasa wakulima kwenye maeneo ya mbali wameweza kuuza mazao yao ya kilimo katika miji mikubwa, jambo ambalo ni muhimu katika kuchochea biashara ya ndani nchini Jamhuri ya Kongo.

Bw. Liwata pia ameishukuru China kutokana na uungaji mkono wake kwa nchi za Afrika ikiwemo Jamhuri ya Kongo kwenye mapambano dhidi ya janga la virusi vya Corona. Amesema, wakati janga hilo lilipolipuka Afrika, China ilitoa misaada mara moja kwa nchi za Afrika. Akiwa mwanahabari, amesema alishuhudia misaada ya vifaa tiba vilivyotolewa na China ikiwasili Jamhuri ya Kongo shehena moja baada ya nyingine, na kwamba ingawa kwa sasa kuna chanjo nyingi za COVID-19 nchini Jamhuri ya Congo, lakini chanjo za China bado zinapendelewa zaidi.

Ushirikiano unaoimarika siku hadi siku kati ya China na Jamhuri ya Kongo umewaleta karibu watu wa nchi hizo mbili. Bw. Liwata amesema, nchini Jamhuri ya Kongo, karibu vijana wote wana hamu ya kujifunza lugha ya Kichina, na karibu wanafunzi wote waliorudi nchini humo baada ya kuhitimu masomo yao nchini China, wamekuwa mabalozi wa urafiki kati ya nchi hizo mbili. Bw. Liwata amesema, sasa watu wa Kongo wanafuatilia mambo ya China, na anatumai kuwa, vyombo vya habari vya China na Jamhuri ya Kongo vitaimarisha zaidi ushirikiano katika siku zijazo, ili kuongeza maelewano kati ya watu wa nchi hizo mbili.