Serikali ya Ethiopia yaruhusu magari yenye misaada ya kibinadamu, na huduma za kibinadamu za usafiri wa anga kwenda Tigray
2021-11-25 08:51:25| CRI

Ofisi ya uratibu wa misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa OCHA imesema kwa mara ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya mwezi mmoja, malori 40 yaliyosheheni misaada ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na chakula, yameruhusiwa kuingia katika jimbo la Tigray nchini Ethiopia.

Malori hayo yaliondoka jumanne kutoka mji wa Semera wa Afar kwenda Tigray, ikiwa ni mara ya kwanza tangu Oktoba 18. Malori hayo pia yamebeba mafuta na dawa na sasa yanasubiri mjini Semera kabla ya kupata ruhusa.

Taarifa iliyotolewa na OCHA inasema kutokana na hali ya Tigray kuendelea kuwa mbaya, ni muhimu kwa misaada hiyo kupelekwa Tigray, na kama ilivyotajwa awali, ni malori 500 yanayohitajika kwa wiki.

Habari pia zinasema huduma za ndege za kibinadamu kuelekea mji wa Mekelle wa Tigray zimeanza tena, baada ya kuzuiwa tangu Oktoba 25.