Uganda yawa nchi ya tatu duniani kwa sera za kudhibiti Tumbaku
2021-11-29 11:00:42| cri

Kituo cha Kimataifa cha Utawala Bora katika Udhibiti wa Tumbaku (GGTC), kimetoa viwango vya utafiti wa Kiashiria cha Kuingilia Sekta ya Tumbaku Duniani 2020 na kuitaja Uganda kuwa nchi ya tatu duniani kwenye juhudi za kudhibiti kwa ufanisi matumizi ya tumbaku, ambapo nafasi ya kwanza imechukuliwa na Brunei ikifuatiwa na Ufaransa.

Kiashiria cha Kuingilia Sekta ya Tumbaku Duniani 2020 ni utafiti unaofanywa duniani juu ya namna serikali zinavyoingilia kati sekta ya tumbaku na kulinda sera za afya ya umma dhidi ya maslahi ya kibiashara ya sekta ya tumbaku kama inavyotakiwa na Shirika la Afya Duniani. Katika Afrika Uganda imekuwa ya kwanza kati ya nchi 14 ikifuatiwa na Kenya ambayo ipo nafasi ya tisa.

Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Kitaifa la Wateja wa Afya la Uganda (UNHCO), Bi. Robinah Kaitirimba, amesema ingawa Uganda imetambuliwa duniani kwa sheria na sera zake thabiti dhidi ya tumbaku, lakini bado kuna pengo linalohitajika kuzibwa.