Watu 20 wauawa katika shambulizi nchini DRC
2021-11-30 08:39:21| CRI

Watu 20 wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika shambulizi lililofanywa dhidi ya kambi ya wakimbizi wa ndani (IDP) nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imesema, shambulizi hilo, karibu na Drodro, eneo la Djugu, jimbo la Ituri, ni la nne linalolenga kambi ya wakimbizi wa ndani.

Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, David McLachlan-Karr, amesema mashambulizi hayo ni ukiukaji wa sheria ya kibinadamu na Mkutano wa Kampala wa mwaka 2009 kuhusu wakimbizi wa ndani. Ametoa wito kwa mamlaka nchini DRC katika ngazi ya taifa na mkoa huo, kuchukua hatua za dharura kulinda raia, ikiwemo wakimbizi wa ndani.