Mawaziri wa mambo ya nje wa China na Tanzania wakutana
2021-12-01 15:57:54| Cri

Waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Wang Yi amekutana na mwenzake wa Tanzania Bibi Liberata Mulamula wakati wa mkutano wa nane wa mawaziri wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika FOCAC mjini Dakar, Senegal.

Bw. Wang amesema urafiki kati ya China na Tanzania umejengwa na kukuzwa na viongozi waasisi wa nchi hizo na rais Xi Jinping wa China aliichukulia Tanzania kama ziara yake ya kwanza barani Afrika baada ya kuingia madarakani, jambo ambalo limeonesha hadhi muhimu ya Tanzania katika diplomasia ya China. China inapenda kuchukulia makubaliano muhimu yaliyofikiwa na viongozi wa nchi hizo mbili kama maelekezo na kutumia fursa ya mkutano huo wa Dakar kama njia ya kujenga uhusiano imara wa China na Afrika.

Bibi Mulamula alipongeza miaka 100 ya kuanzishwa kwa Chama cha Kikomunisti cha China CPC na miaka 50 ya kurejeshwa kiti halali cha Jamhuri ya Watu wa China kwenye Umoja wa Mataifa na pia kupongeza hatua kubwa zilizotangazwa na rais Xi kwenye ufunguzi wa mkutano wa Dakar. Alisema Tanzania na China ni marafiki wazuri, wa kweli na Tanzania inapenda kuimarisha mshikamano na urafiki wake na China, kuendelea kuunga mkono China kwenye masuala yanayohusu maslahi makuu na ufuatiliaji mkubwa wa China. Pia Tanzania inatarajia kuimarisha ushirikiano na China katika miundombinu na biashara, kubadilishana maoni kwenye utawala wa nchi ili kutimiza maendeleo mazuri ya Tanzania.