IGAD na FAO yatoa wito wa kuchukuliwa hatua za kukabiliana na athari za ukame katika pembe ya Afrika
2021-12-01 12:19:28| cri

Shirika la Maendeleo ya Serikali za nchi za Afrika Mashariki (IGAD) na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) yametoa wito wa kuchukuliwa hatua haraka za kukabiliana na athari za ukame katika pembe ya Afrika ambako hali ya uhaba wa chakula inazidi kuwa mbaya.

Kwenye taarifa iliyotolewa kwa pamoja na Katibu mtendaji wa IGAD Workneh Gebeyehu na Mratibu wa FAO wa kanda ya Afrika Mashariki Chimimba David Phiri, inasema msimu wa mvua wa mwezi Oktoba hadi Disemba 2021 umechelewa sana katika kanda hiyo, ambapo maeneo mengi yana mvua chache au hayana kabisa. Ukame mkali unakadiriwa kusababisha kuzorotesha kilimo na malisho ya wanyama, na kupelekea kaya ambazo tayari zinataabika na hatari nyingi na za wakati mmoja zikiwemo mabadiliko ya hali ya hewa, migogoro, COVID-19, na nzige wa jangwani kupunguza matumizi yao ya chakula.

Hadi kufikia Oktoba 2021, watu milioni 26 katika kanda hiyo tayari walikuwa wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na kutokana na tishio la hali ya ukame kuwa mbaya zaidi, uhaba wa chakula unaweza kuongezeka katika nusu ya kwanza ya mwaka 2022 katika pembe ya Afrika.