Umoja wa Afrika wakaribisha ahadi zilizotolewa na China kwenye mkutano wa FOCAC Senegal
2021-12-02 08:51:00| CRI

Shirika la Maendeleo la Umoja wa Afrika lenye makao yake makuu mjini Johannesburg (AUDA-NEPAD), limekaribisha ahadi zilizotolewa na China kusaidia Afrika kwa chanjo na uwekezaji, na kusainiwa kwa nyaraka nne za kimkakati.

Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa AUDA-NEPAD Bw. Ibrahim Mayaki, alisema hayo jana kwenye mkutano wa kujadili matokeo ya Mkutano wa 8 wa Mawaziri wa baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC). Amesema ahadi iliyotolewa na China kuhusu chanjo ya COVID-19 inakaribishwa, ikiwa ni ishara ya mshikamano na Afrika katika mapambano dhidi ya janga la COVID 19, na aina mpya ya virusi vya Omicron.

Hadi kufikia Novemba 12, China ilikuwa imetoa zaidi ya dozi bilioni 1.7 za chanjo ya COVID-19 kwa zaidi ya nchi na mashirika 110, zikiwemo nchi 50 za Afrika na tume ya Umoja wa Afrika. Kenye mkutano huo China ilitangaza kuwa itatoa dozi nyingine bilioni 1 za chanjo ya COVID-19 kwa nchi za Afrika ili kusaidia kufikia lengo la Umoja wa Afrika la kuchanja asilimia 60 ya watu ifikapo mwaka 2022.

Wakati wa mkutano huo China iliahidi kuwa itatoa dola bilioni 10 ili kuhimiza biashara na mauzo ya nje ya Afrika, na kuwekeza dola bilioni 10 za kimarekani barani Afrika katika miaka mitatu ijayo.