China na Tanzania ziko tayari kuimarisha uhusiano kati yao
2021-12-02 08:51:46| CRI

Waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Wang Yi, na mwenzake wa Tanzania Bibi Liberata Mulamula jana walifanya mazungumzo mjini Dakar, Senegal na kusema nchi zao tayari kuimarisha uhusiano kati yao.

Kwenye mkutano wao uliofanyika kando ya mkutano wa 8 wa Mawaziri wa Baraza la Ushrikiano kati ya China na Afrika, Bw. Wang amesema urafiki kati ya China na Tanzania ulianzishwa na viongozi waasisi wa pande hizo mbili na umekua na kuimarika kadiri muda unavyosonga mbele.

Amekumbusha kuwa kutokana na umuhimu wa Tanzania kwenye diplomasia ya China na Afrika, Rais Xi Jinping aliichagua Tanzania kuwa kituo cha kwanza cha ziara yake barani Afrika baada ya kuingia madarakani. Amesema China iko tayari, chini ya mwongozo wa makubaliano muhimu yaliyofikiwa na wakuu wa nchi hizo mbili, kuuchukulia mkutano wa Dakar kama fursa ya kuendeleza uhusiano usioweza kuvunjika kati ya China na Tanzania.

Bibi Mulamula ametoa pongezi za dhati kwa maadhimisho ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na mwaka wa 50 wa kurejeshwa kwa kiti halali cha Jamhuri ya Watu wa China katika Umoja wa Mataifa, na pia alikaribisha kwa moyo mkunjufu mipango muhimu iliyotangazwa na Xi kuhusu ushirikiano na Afrika kwenye ufunguzi wa mkutano wa Dakar.