Afrika yaimarisha upimaji wa virusi vya Omicron huku idadi ya walioambukizwa kusini mwa Afrika ikizidi kuongezeka
2021-12-03 08:46:39| CRI

Afrika yaimarisha upimaji wa virusi vya Omicron huku idadi ya walioambukizwa kusini mwa Afrika ikizidi kuongezeka_fororder_VCG111359425664

Shirika la Afya duniani WHO limesema nchi za Afrika zimeimarisha hatua za upimaji na udhibiti wa virusi vya COVID-19 aina ya Omicron huku maambukzi ya virusi hivyo yakiongezeka kwa asilimia 54 katika eneo hilo.

Mpaka sasa virusi aina ya Omicron vimeripotiwa katika nchi nne za Afrika, ambazo ni Botswana, Afrika Kusini, Ghana na Nigeria, na nchi nyingine zaidi ya 20 duniani zimegundua uwepo wa virusi hivyo. Ofisi ya WHO kanda ya Afrika yenye makao yake mjini Brazzaville imesema Botswana na Afrika Kusini zinachukua asilimia 62 ya maambukizi yote ya virusi hivyo duniani.

Ofisi hiyo imesema kuna uwezekano aina ya virusi vya Omicron vikagunduliwa katika nchi nyingi zaidi, kwa hiyo mamlaka za kitaifa zimeongeza shughuli za ufuatiliaji

WHO imeonya kuwa kutokana na viwango vya chini vya utoaji wa chanjo barani Afrika, kuna hatari ya virusi hivyo kuenea zaidi. Hadi sasa ni watu milioni 102 tu, au asilimia 7.5 ya watu wote barani Afrika ndio wamepatiwa chanjo kikamilifu. Zaidi ya asilimia 80 ya watu bado wanahitaji kupokea dozi ya kwanza.