Kutumia madawa vizuri na ushauri vimenisaidia kuishi maisha ya kawaida licha ya kuambukizwa HIV
2021-12-03 20:25:29| cri

Na Ronald Mutie

Edith Nyambura ni mama wa watoto wawili haoni haya wala kuogopa kuelezea hali yake ya HIV.

Alifahamu kuwa ana virusi vya HIV kuanzia mwaka wa 1998, lakini alianza kutumia dawa mara moja na kupata ushauri nasaha kuhusu jinsi ya kuishi na virusi hivyo.

Wakati dunia ikiadhimisha siku ya ukimwi duiani Desemba 1, yeye amekuwa miongoni mwa wanaharakati wa kuhamasisha jamii kwa jumla kwamba  virusi hivyo sio mwisho wa maisha.

“Nilipoambiwa nina virusi kwanza haikuwa rahisi kukubali, kwa sababu watu walikuwa wanasema ugonjwa huo hauna dfawa na mtu anaweza kufa ndani ya hata siku chache tu, lakini sio kweli hayo ni mawazo tu ya watu”, anasema Nyambura.

Sasa Nyambura ana watoto wawili na hawana virusi hivyo na wanaendelea na masomo yao.

Mwaka 2011 alianzisha kikundi cha kutoa ushauri kwa kina mama ambao wameathirika jinsi ya kuishi maisha ya kawaida na kuwaepusha na unyanyapaa.

“Kinachonipa nguvu kila siku ni kuona mtu ambaye ameathirika amepata ushauri na hajapitia maisha magumu yaani amekubali hali yake na anakunywa dawa”, anasema Nyambura.

Juhudi za mama Nyambura pia zinapata uuungwaji mkono na mashirika kama vile Mtandao wa Kitaifa wa Uwezeshaji wa Watu Wanaoishi na HIV -NEPHAK.

NEPHAK inashirikisha vikundi vya watu wote nchini Kenya wanaoishi na virusi vya HIV.

Afisa wa NEHPAK Queenter Muguiru anasema kazi zao ni pamoja na kutoa ushauri kwa waathiriwa kuhusu utumiaji wa dawa, kuwapa habari husika ya jinsi ya kuendelea kuishi maisha ya kawaida na kujiepusha na mambo yanayoweza kuongezea hatari za kiafya.

Kwa mujibu wa takwimu za Baraza la Taifa la Kudhibiti Ukimwi nchini Kenya, maambukizi mapya yamepungua kwa asilimia 68.4 kati ya 2013 na 2021.

Akiongoza sherehe ya kuadhimisha siku ya Ukimwi duniani, Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amesema nchi hiyo imepata mafanikio makubwa katika kupunguza kasi ya kuenea kwa HIV katika miaka ya hivi karibuni.

Katika kipindi hicho yaani 2013-2021, Uhuru alisema vifo vinavyotokana na VVU/UKIMWI vimepungua kwa asilimia 67 kutoka watu 58,446 mwaka 2013 hadi 19,486 mwaka huu.

Rais Kenyatta i alihusisha upunguvu huo na uwekezaji wa serikali katika utafiti, upimaji, kuzuia na kudhibiti VVU/UKIMWI na magonjwa yanayohusiana.

Virusi vya Ukimwi bado vinasalia  kuwa tishio  kwa  afya ya umma na viinaathiri mamilioni ya watu ulimwenguni kote.

Ingawa ulimwengu umepata maendeleo makubwa katika miongo ya hivi karibuni, malengo muhimu ya kimataifa kwa 2020 hayakufikiwa.

Taakwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya watu milioni 37 kote duniani wanaishi na virusi vya ukimwi na kulikuwa namambukizi milioni moja na nusu mwaka 2020 pekee.

Umoja wa mataifa bado unaoa kuwa hakuna usawa katika vita dhidi ya HIV hasa wakati huu dunia inapambanana janga la Covid-19.

Maudhui ya maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani mwaka huu yamekuwa ni “Komesha ukosefu wa usawa. Komesha UKIMWI” ambapo Shirika la afya duniani  WHO na washirika wake wanaangazia ukosefu wa usawa unaoongezeka katika upatikanaji wa huduma muhimu za Virusi vya Ukimwi.

WHO inatoa wito kwa viongozi wa kimataifa na wananchi kukusanyika ili kukabiliana na ukosefu wa usawa unaochochea UKIMWI na kufikia watu ambao kwa sasa hawapati huduma muhimu za kukabili ugonjwa huo.