UM wataka kuzuia unyanyasaji wa kijinsia kaskazini mwa Ethiopia
2021-12-08 08:57:11| cri

Afisa wa Umoja wa Mataifa Jumanne aliitaka serikali ya Ethiopia kutia saini mara moja makubaliano na Umoja huo ili kuzuia unyanyasaji wa kijinsia unaohusiana na mgogoro.

Pramila Patten, mwakilishi maalum wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia unyanyasaji wa kijinsia katika mgogoro, alisema ukatili uliokithiri na unyanyasaji wa kijinsia umekuwa alama kuu za mgogoro katika eneo la Tigray nchini Ethiopia.

Kwenye taarifa yake, Patten ameeleza wasiwasi wake mkubwa kuwa kufuatia kuongezeka na kuenea kwa uhasama na hali ya kibinadamu kuzidi kuwa mbaya katika mikoa ya Tigray, Amhara na Afar, ripoti zinazoendelea kusikika kuhusu mashambulizi dhidi ya wanawake, wasichana, wavulana na wanaume, ikiwa ni pamoja na ukatili wa moja kwa moja wa kijinsia kama silaha kwenye vita kwa njia ya kulipiza kisasi, adhabu, udhalilishaji, na pia kuwanyanyapaa watu kulingana na utambulisho wao halisi au wanaodhaniwa wa kikabila.

Ametoa wito kwa pande zote kwenye mgogoro kusitisha mara moja kila aina ya unyanyasaji wa kijinsia na kukomesha uhasama ili kuandaa njia za kufanya juhudi za kusitisha mapigano na kujenga amani kwa pamoja kwa lengo la kuhimiza ujumuishi na usawa wa kijinsia.