Benki ya Dunia yasema kilimo cha kihaidroponiki na ufugaji wa wadudu katika Afrika ndio jibu la kukabiliana na ukosefu wa chakula
2021-12-09 12:28:50| cri

Benki ya Dunia imesema kwenye ripoti yake kwamba kutumia zaidi kilimo cha kihaidroponiki yaani kupanda mimea bila udongo pamoja na ufugaji wa wadudu katika Afrika linaweza kuwa ndio jibu la kukabiliana na njaa, umasikini na msukosuko wa kiikolojia.

Ripoti hiyo iliyopewa jina la “Ufugaji wa Wadudu na Kilimo cha kihaidroponiki katika Afrika: Mzunguko Mpya wa Uchumi wa Chakula” imesema mifumo hiyo miwili mipya ya uzalishaji chakula inaweza kustawi katika bara la Afrika ambalo linaendelea kukabiliwa na uhaba wa maji na kupungua kwa ardhi ya kilimo. Kwa mujibu wa makamu wa rais wa Benki ya Dunia anayeshughulikia maendeleo endelevu Juergen Voegele, njia hizo zinaweza kuleta ajira, kubadilisha maisha, kuboresha lishe na kuleta faida nyingine nyingi katika Afrika na nchi zilizoathirika na migogoro.

Ripoti hiyo iliyokusanywa katika nchi 13 za Afrika zikiwemo zile zilizoathirika na migogoro, imesema ufugaji wa wadudu na kilimo cha kihaidroponiki kinaweza kusaidia kutatua masuala ya utapiamlo unaoathiri moja ya tano ya watu wa Afrika.