Katibu mkuu wa UM alaani shambulizi dhidi ya timu ya UNHCR nchini DRC
2021-12-09 12:27:46| cri

Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Stephane Dujarric amesema, Bw. Antonio Guterres amelaani vikali shambulizi lililofanywa jana na waasi wa Mai-Mai dhidi ya timu ya Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) mkoani Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Msemaji huyu amesema timu hiyo iliyokuwa ikisindikizwa na tume ya Umoja wa Mataifa nchini DRC (MONUSCO) ilishambuliwa ikiwa njiani wakati inarudi mji wa Beni baada ya kutoa msaada wa kibinadamu kwa wakimbizi, na wafanyakazi watatu wa UNHCR walijeruhiwa kwenye shambulizi hilo. Katibu mkuu wa UM ametoa wito kwa DRC ifanye uchunguzi kadri iwezekanavyo, na kuwawajibisha wanaohusika.

Wakati huohuo, Guterres amelaani vikali shambulizi la jana dhidi ya msafara wa magari wa tume ya Umoja wa Mataifa nchini Mali, ambalo limesababisha vifo vya askari saba wa kulinda amani wa Togo, na wengine watatu wamejeruhiwa vibaya.